Nafasi Ya Matangazo

August 09, 2026



Na WMA - DODOMA.
Wakala wa Vipimo (WMA) umemhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mhe. Selemani Mwendwa kuwa utaongeza kasi ya utendaji kazi wa masuala ya vipimo katika wilaya hiyo ili kulinda uchumi wa wakulima na wafugaji.

Hakikisho hilo limetolewa jana Agosti 8, 2026 alipotembelea banda la WMA kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane, Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Dodoma, na kupatiwa elimu ya vipimo.

Meneja wa WMA Mkoa wa Singida, Bw.  Willie Amosi alisema kuwa "WMA itashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuratibu na kutoa elimu ya vipimo katika maeneo mbalimbali ya Iramba kwa  lengo la kufikia wakulima wa mahindi, alizeti na pamba pamoja na wafugaji kwenye minada na masoko.

Aidha,  alimjulisha  Mkuu wa Wilaya kuwa WMA  itajipanga ili  kuanzisha Klabu za Vipimo (Vipimo Clubs) katika shule mbalimbali  za msingi na sekondari ikiwa ni mikakati ya kufika Tanzania nzima, hususan Tanzania Bara ambao ndiyo uwanda wa WMA. 

Vilevile, Meneja Amosi alisema kuwa WMA itaendelea  kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili wananchi wa Iramba waweze kuripoti moja kwa moja matumizi ya vipimo visivyo rasmi vinavyotumika katika masoko  na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa uharaka

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya alisema:  
“Nimefurahishwa sana. Kama Serikali ya Wilaya tuko tayari kushirikiana na WMA ili kuhakikisha vipimo sahihi vinatumika na wananchi waweze kupata stahiki ya jitihada zao. Ningetamani Iramba iwe miongoni mwa   Wilaya zinazotumia vipimo sahihi katika sekta za kilimo.uvuvi pamoja na ufugaji.”

Wataalamu wa WMA walimkabidhi pia vipeperushi vyenye elimu ya vipimo ili vimsaidie kuendelea kujenga uelewa wa elimu ya vipimo.
Posted by MROKI On Sunday, August 09, 2026 No comments



Na WMA - DODOMA.
Kiongozi mstaafu wa Wakala wa Vipimo (WMA), aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bw. Deogratius Aloyce Maneno amesema uwekezaji wa Serikali katika masuala ya vipimo ndiyo ufunguo wa kujenga uchumi imara na soko la haki.

Alisema hayo jana Agosti 8, 2026 alipotembelea banda la WMA kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima (Nane Nane), yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Dodoma.

Baada ya kupokelewa na wataalamu wa WMA na kupewa maelezo ya maboresho mapya ya vifaa na elimu ya vipimo, Mkurugenzi Mstaafu alisema anajivunia kuona kazi aliyoshiriki kuianzisha ikiendelea na kukua.

“Nimefurahishwa sana kuona WMA imepiga hatua kubwa. Tulipoanza tulikuwa na changamoto za vifaa na uelewa, lakini leo naona vijana wanasimama wenyewe kutoa elimu. Hii ndiyo tija ya uwekezaji,” alisema.

Kutokana na uzoefu wake wa miaka mingi WMA, kiongozi huyo alitoa ushauri katika maeneo kadhaa ili kuboresha zaidi huduma za uhakiki wa vipimo.

 Kwanza, alisema kuwa ni jambo jema kutoa elimu kwa wafanyabiashara wakubwa. Hata hivyo alisisitiza kuwa "huu ni wakati wa kushuka ngazi hadi kwa mama lishe na wauuzaji wa sokoni maana ndio wanaoumia zaidi na vipimo visivyo rasmi,” alisema.

Pia, 'Bosi Deo' kama wengi wanavyomwita alitoa ushauri kwa wafanyabiashara kukumbatia teknolojia akisema kuwa “Dunia imebadilika. Tumieni mizani ya kidijitali zaidi na mifumo ya kutoa risiti. Hii itasaidia kuwa na rekodi na kupunguza ubadhilifu katika biashara.”

Aidha, alitoa ushauri kwa watendaji wa WMA kutokuogopa kutumia sheria inayoingoza Wakala kuwabana wale wanaokiuka maelekezo na taratibu halali za kivipimo. 

“WMA ina mamlaka. Itumieni. Mkikamata na kutoa faini kwa wale wanaokiuka, wengine watafuata sheria. Soko la haki linahitaji nidhamu.”

Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa WMA, Bi. Veronica Simba, alimshukuru kiongozi huyo mstaafu kwa kuwa sehemu ya walioweka misingi imara ya utendaji kazi WMA.

“Tunajivunia alama ambayo wewe pamoja na wastaafu wengine mliiweka. Leo tunaendeleza dira yenu ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata kipimo sahihi. Milango yetu iko wazi kwa ushauri wako wakati wote,” alisema.

Wananchi waliokuwepo bandani walifurahishwa na uwepo wa kiongozi huyo mstaafu na kusema ni mfano mzuri wa watu kurejea kutoa uzoefu kwa vizazi vipya.

Wastaafu wengine waliotembelea banda la WMA kwenye Maonesho ya NaneNane ni pamoja na Bw. Evarist Masengo aliyekuwa Meneja wa WMA ngazi ya Mkoa na Bw. Joseph Maliti aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi. Wote walikiri kufurahishwa na maendeleo ya Wakala na waliupongeza Uongozi uliopo pamoja na wafanyakazi wote kwa ujumla.
Posted by MROKI On Sunday, August 09, 2026 No comments



Na WMA - DODOMA.
Meneja wa Fedha wa Wakala wa Vipimo  (WMA), Bw. Ibrahim Mbinga, amesema usimamizi mbovu wa vipimo ndiyo adui mkubwa wa mfuko wa mfanyabiashara, mkulima na mnunuzi.

Akizungumza na wadau katika banda la WMA kwenye Maonesho ya 33 ya Nane Nane, Dodoma, Agosti 8, 2026 Meneja huyo amefafanua jinsi vipimo visivyo rasmi vinavyosababisha upotevu wa fedha usioonekana.

Mbinga ameeleza kuwa majukumu ya WMA yanalenga kuokoa wafanyabiashara, wakulima na walaji. “Watu wengi wanafikiri kupima kwa ndoo au visado ni rahisi. Lakini ukweli ni kwamba unajipiga risasi mguuni. Kila kilo, kila lita iliyopotea ni shilingi iliyotoka mfukoni mwako,” alisema.

Akidadavua kuhusu hesabu ya fedha kwenye vipimo, alisema vipimo ni sawa na mfuko wa fedha. “Gunia la mahindi kilo 100 ukiuza kwa ndoo 18 badala ya mizani, unapoteza kilo 10. Kama gunia ni shilingi 100,000, umepoteza shilingi 10,000. Ukiuza magunia 10 kwa wiki, umepoteza shilingi 100,000. Kwa mwezi ni milioni 1.2. Hiyo pesa ingekuwa wapi?” aliuliza.

Akieleza zaidi, alisema kuwa wafanyabiashara wengi hulalamika kupata hasara lakini akafafanua kuwa 'unaponunua mafuta lita 19 badala ya 20, au mpunga kilo 18 badala ya 20, unalipa pesa kamili na kupata bidhaa pungufu. Hiyo ni hasara ya moja kwa moja."

Akizungumzia mikopo kutoka Benki kwa wafanyabiashara wakulima alisema "Benki leo haziombi tu dhamana bali zinataka rekodi. Mkulima anayetumia mizani iliyohakikiwa na kuwa na risiti anaaminika zaidi. Vipimo sahihi vinakupa historia ya biashara yako ambayo benki inaitaka."

Aidha, Mbinga pia aliwaelimisha wafanyabiashara wakulima kuepuka gharama za faini ambazo husababisha hasara.

Akifafanua, alisema "kutumia vipimo visivyo rasmi ni kosa kisheria. Unapokamatwa unalipa faini na wakati mwingine bidhaa inaweza kuzuiliwa hivyo ni hasara mbili kwa wakati mmoja.

Badala yake, aliwashauri kuwekeza kiasi kidogo cha pesa kununua mizani iliyohakikiwa na WMA ili kujiepusha  na faini inayoweza kukuletea hasara.

Katika hatua nyingine, Mbinga aliwashauri wafanyabiashara wakulima 'kujenga jina' ili kupata faida stahiki. "Mteja anapojua kuwa kwako anapata haki yake, atarudi tena na tena na ataleta wengine. Hiyo inakupunguzia gharama ya kutafuta wateja. Uaminifu unalipa," alisisitiza.

Meneja huyo wa Fedha, alihitimisha kwa kusisitiza kaulimbiu ya WMA isemayo "Pima kwa Haki, Pata Faida Halali" akidadavua kuwa mfanyabiashara  akiwekeza kwenye mizani iliyohakikiwa leo, baada ya miezi miwili atashangaa tofauti yake kwenye akaunti yake ya fedha. 

Mbinga amewataka wadau pia kutumia risiti na vitabu vya mauzo vinavyotokana na vipimo sahihi ili kufuatilia kwa urahisi mapato na matumizi.

Kwa upande wao, Wadau wameipongeza WMA kwa kuleta wataalamu wa fani mbalimbali katika banda la maonesho ya Nane Nane na kusema elimu ya kifedha imewapa uelewa mpya.
Posted by MROKI On Sunday, August 09, 2026 No comments

August 08, 2026

Na Mwandishi Wetu
JAMII ya Wandondi na Wandwewe, imetoa mwito wa kitaifa na kimataifa kwa watu wote wenye nia njema kuungana katika Dua Maalum kwa ajili ya Amani, Umoja, Maridhiano, Mshikamano na Ulinzi wa Maisha ya Binadamu.

Dua hiyo ni mwito wa pamoja unaolenga kuwakutanisha watu wa imani, mila, tamaduni na mitazamo mbalimbali katika kusimama kwa pamoja Na Mwandishi Wetu amani, utu, uhai, mshikamano na heshima kwa mwanadamu, bila kujali tofauti za dini, kabila, rangi, taifa, utamaduni, itikadi au hali ya kijamii.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Chifu Felix G. L. Mfunda, kwa niaba ya jamii ya Wandondi na Wandwewe amesema dua hiyo itafanyika  Agosti 12, 2026,  ambapo Misa Maalumu ya Kikatoliki itafanyika katika Kanisa Katoliki, Kigango cha Mhangazi, Parokia ya Kitanda, Namtumbo, Ruvuma. huku akitoa  mwito wa amani na maridhiano.

Aidha, kuanzia jioni ya Agosti 13 hadi mchana wa Agosti 14, 2026, kutafanyika dua, na shughuli za jadi zitakazoambatana na ngoma na sanaa mbalimbali za asili za Wandwele na Wandondi.

Jamii mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma, zikiwemo Makumbo, Lizombe na Makiwa, zinatarajiwa kushiriki katika shughuli hizo zinazolenga kuenzi urithi wa tamaduni, kuimarisha undugu na mshikamano, pamoja na kukuza amani kati ya jamii.

Mfululizo huo utakamilishwa Agosti 16, 2026, kwa Dua Maalumu ya Kiislamu itakayofanyika jioni kwa ajili ya kuiombea Tanzania, Afrika na dunia nzima.
Ambapo  amesema Dunia ya leo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo migogoro, vita, chuki, migawanyiko ya kijamii, changamoto za kiuchumi, ukosefu wa usawa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Katika mazingira haya, tunapaswa kutambua kwamba amani si wajibu wa Serikali pekee; ni wajibu wa kila mwanadamu.Tunatoa mwito kwa viongozi wa kitaifa na kimataifa, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, wasomi, vijana, wanawake, mashirika ya kiraia na wananchi wote kutumia nafasi zao kujenga madaraja ya maelewano badala ya kuta za migawanyiko.

“Tunasisitiza umuhimu wa mazungumzo, kusikilizana, kusameheana, kuheshimiana na kutafuta suluhu za amani katika kila tofauti inayojitokeza.”

Aidha amesema ulinzi wa maisha ni wajibu wa pamoja akifafanua maisha ya mwanadamu ni tunu kubwa na hayapaswi kuwekwa rehani kwa sababu ya tofauti za kisiasa, kidini, kikabila, kiuchumi, kijamii au kiitikadi.

Ameongeza kwa msingi huo, wanatoa mwito wa kuheshimiwa kwa utu wa binadamu, haki ya kuishi, usalama wa raia na ulinzi wa watoto, wanawake, wazee na makundi yote yaliyo katika mazingira hatarishi.

“Tunasisitiza tofauti zetu zisigeuke kuwa sababu ya kupoteza maisha ya watu.Kila jamii ina wajibu wa kulinda maisha na kujenga mazingira ambayo kila mwanadamu anaweza kuishi kwa usalama.

Pia amesema kuhusu amani, afya na ulinzi wa mazingira ni kwamba amani ya kweli haiwezi kutenganishwa na afya ya jamii, usalama wa chakula, maji safi, mazingira salama na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.

“Uharibifu wa mazingira, ukataji wa misitu, uharibifu wa vyanzo vya maji, upotevu wa bayoanuai na athari za mabadiliko ya tabianchi vinaweza kuongeza changamoto za kijamii na kiuchumi na kuhatarisha maisha ya watu.

“Kwa hiyo, tunatoa mwito wa kuunganisha juhudi za amani, afya, mazingira na maendeleo endelevu kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Akieleza zaidi amesema katika dua kwa Watanzania ,Afrika na Dunia amefafanua Tanzania iendelee kuwa taifa la amani, umoja, mshikamano na utulivu na kwa Afrika ipate amani na utulivu wa kudumu.

Pia migogoro na vita duniani zipungue na hatimaye kumalizika na kuongeza viongozi wapate hekima, busara, uadilifu na moyo wa kuhudumia watu.Vijana wapate fursa za elimu, ajira, ubunifu, ujasiriamali na maendeleo.

Kwa watoto walindwe dhidi ya ukatili, unyanyasaji na mazingira yanayohatarisha maisha yao. Wanawake, wazee na makundi yaliyo katika mazingira magumu walindwe na kuheshimiwa.Wagonjwa na wote wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali wapate faraja, matumaini na huduma stahiki na mazingira.

Kuhusu ujumbe kwa Watanzania amesema wanawakumbusha Umoja wetu ni nguvu yetu, amani yetu ni utajiri wetu, na maisha ya kila Mtanzania ni sehemu ya thamani ya Taifa letu.

“Tunapaswa kukataa chuki, uchochezi, ubaguzi, vurugu na lugha zinazogawa jamii. Badala yake, tujenge utamaduni wa kusikilizana, kuheshimiana, kusameheana, kusaidiana na kutatua tofauti zetu kwa njia za amani.

“Tanzania yenye amani na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya watu wake na mchango mkubwa kwa amani ya Afrika na dunia.”

 


Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments




DODOMA
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, amesema Maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu la kuwaelimisha wananchi kuhusu Sekta ya Madini, kusikiliza maoni yao na kupata mrejesho unaosaidia kuboresha huduma na kuongeza thamani ya sekta hiyo.

Mhandisi Swedi amesema hayo baada ya kutembelea mabanda ya Taasisi za Wizara ya Madini katika kilele cha Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma, akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika maendeleo ya sekta hiyo.

Amesema maonesho hayo yanawezesha Tume ya Madini kuwafikia wananchi moja kwa moja, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kupata maoni ambayo yanaweza kutumika kuboresha utendaji na utoaji wa huduma.

“Kila swali na hoja inayotolewa na mwananchi ni muhimu, kwa sababu inatusaidia kutambua maeneo yanayohitaji maboresho na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma,” amesema Mhandisi Swedi.

Aidha, amesema ushiriki wa wananchi katika Maonesho ya Nanenane unaimarisha ushirikiano kati ya Serikali, taasisi zinazohusika na Sekta ya Madini na jamii, sambamba na kuwawezesha wananchi kupata uelewa kuhusu huduma, fursa na shughuli mbalimbali zinazopatikana katika sekta hiyo.

Katika ziara hiyo, Mhandisi Swedi ametembelea mabanda ya Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), ambako amepata fursa ya kujionea huduma na shughuli zinazotekelezwa na taasisi hizo.

Amewahimiza wananchi kutumia kikamilifu fursa inayotolewa na Maonesho ya Nanenane kwa kujifunza, kuuliza maswali na kutoa maoni kuhusu Sekta ya Madini.

Pia, amewakaribisha wananchi kufika katika ofisi za Tume ya Madini na taasisi nyingine zinazohusika na sekta hiyo ili kupata ufafanuzi na huduma zaidi kuhusu masuala ya madini.
Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments
Na WMA - DODOMA
WAKALA wa Vipimo  (WMA) umewataka wafanyabiashara na wananchi kuacha mara moja matumizi ya vipimo visivyo rasmi, ikiwemo ndoo, mafungu, visado na makopo, katika uuzaji wa mazao ya kilimo na mifugo na badala yake kutumia mizani iliyohakikiwa kwa mujibu wa sheria.

Wito huo umetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihula, leo Agosti 8, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Siku ya Wakulima Nane Nane, yaliyokuwa yakifanyika katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, jijini Dodoma.

Kihula amesema matumizi ya vipimo visivyo rasmi yanaweza kusababisha kutokuwepo kwa usawa katika biashara na kuwaathiri wananchi kwa kuwafanya wasipate thamani halisi ya bidhaa wanazonunua au kuuza.

Amesema WMA imeendelea kutoa elimu kwa wananchi, wakulima, wafugaji na wafanyabiashara kuhusu matakwa ya Sheria ya Vipimo, Sura ya 340, ikiwemo namna ya kutambua vipimo vilivyohakikiwa na uwekaji wa alama sahihi kwenye bidhaa zilizofungashwa.

“Ili kuwa na soko lenye haki na kuongeza tija kuelekea Dira ya 2050, hakuna soko linaloweza kuwa la haki bila matumizi ya vipimo vilivyohakikiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Kihula.


Akizungumzia sekta ya kilimo, Kihula amewataka wakulima kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi katika hatua zote za uzalishaji na biashara, kuanzia uandaaji wa mashamba hadi uvunaji, uhifadhi na uuzaji wa mazao.

Amesema matumizi ya vipimo sahihi katika kujua ukubwa wa eneo la shamba yanaweza kusaidia wakulima kupanga uzalishaji kwa usahihi badala ya kutegemea makadirio.

Aidha, amewataka kuhakikisha mazao yanapimwa kwa mizani iliyohakikiwa wakati wa kuuza ili mkulima aweze kupata thamani halisi ya bidhaa zake.

Kwa upande wa wafugaji, Kihula amewataka kuacha kuuza mifugo kwa kutegemea makadirio ya macho na badala yake kutumia mizani sahihi katika kubaini uzito wa mifugo kama vile ng'ombe, mbuzi, kondoo na kuku.

Amesema utaratibu huo unapaswa pia kuzingatiwa katika uuzaji wa bidhaa zinazotokana na mifugo, ikiwemo nyama na maziwa, ili kuhakikisha mnunuzi na muuzaji wanapata thamani inayolingana na kiasi cha bidhaa kinachouzwa.


Wakati huohuo, Kihula amewapongeza wavuvi kwa kuendelea kuonesha mfano mzuri katika matumizi ya vipimo na kuwataka kuendeleza utaratibu huo.

Amesema matumizi ya vipimo sahihi katika shughuli za uvuvi ni muhimu katika kuhakikisha biashara inafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia thamani halisi ya bidhaa.


Kihula amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele kukataa kuhudumiwa kwa vipimo visivyo rasmi wanaponunua bidhaa kama vile viazi, bamia, vitunguu na nyanya, badala yake kusisitiza bidhaa hizo zipimwe kwa mizani iliyohakikiwa.

“Wananchi wasikubali kununua bidhaa kwa mafungu, visado au vipimo vingine visivyo rasmi. Wanapaswa kusisitiza kupimiwa kwa mizani iliyohakikiwa ili kuhakikisha wanapata kiasi sahihi cha bidhaa wanacholipia,” amesema.

Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa kwa WMA wanapobaini matumizi ya vipimo visivyo halali katika maeneo yao ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Amesema ushirikiano wa wananchi, wafanyabiashara na taasisi za Serikali ni muhimu katika kujenga soko lenye haki, uwazi na linalozingatia matumizi ya vipimo sahihi kwa mujibu wa sheria.

Amesisitiza kuwa matumizi ya vipimo vilivyohakikiwa si suala la wafanyabiashara pekee, bali ni jambo linalomhusu kila mwananchi katika kuhakikisha anapata thamani halisi ya fedha anayolipa au mapato anayopata kutokana na bidhaa anazouza.



Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments




Na Neema Chalila Mbuja, DodomaRAIS  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 8, 2026 amefunga rasmi Maonesho ya NANE NANE  yaliyokuwa yakifanyika kwenye Viwanja vya Dkt John Malecela  Nzuguni Dodoma na kuwapongeza Wizara ya Kilimo , Mifugo na Uvuvi kwa kazi nzuri liliyofanya kuwaunganisha wadau wa kilimo kwenye maonesho hayo.

Katika Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii maelfu ya wananchi wamefurika kwenye bustani ya wanyamapori hai ili kujionea wanyama mbalimbali.

Sambamba na hilo viongozi mbalimbali wa Wizara ya Maliasili na Utalii wametembelea banda la Wizara hiyo kwenye Viwanja vya NANE NANE kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika na taasisi na wadau wa   Malikale, Misitu na Nyuki, Utalii na Wanyamapori.

Wakiwa kwenye Maonesho hayo walipata fursa ya kuzungumza na wananchi na wadau na kueleza mustakabali wa sekta ya utalii sambamba na mikakati iliyojiwekea kwa ajili ya kutangaza sekta ya utalii hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.






Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Taasisi za Dini ambazo kwa namna ya pekee zimekuwa zikishiriki katika kutoa mchango kwenye sekta za Afya na Elimu hapa nchini.
 
Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu Maalum ya Wanajumuiya wa Uru Seminari, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Kristo Mchungaji Mwema – Tabata Kimanga Jijini Dar es Salaam. Amesema kwa miaka mingi na kwa asilimia kubwa Taasisi za dini zimechangia katika utoaji wa huduma za elimu na afya, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi hizo ili kufanikiwa zaidi katika kulijenga Taifa.
 
Makamu wa Rais amesema Malezi yanayotolewa katika Taasisi za elimu za dini ikiwemo Shule ya Uru Seminari ambayo husisitiza Sala, Kazi na Masomo yanapaswa kutiliwa mkazo katika malezi ya vijana wa sasa. Amesema vijana watakavyoweza kumjua Mungu, kufanya kazi kwa bidii pamoja na kupata elimu wataweza kulijenga vema Taifa kupitia ujuzi na hivyo kuepusha tabia za kupata kipato kupitia njia zisizo sahihi.
 
Makamu wa Rais amewashukuru, walimu, walezi na wanafunzi waliopata elimu Uru Seminari kwa ushirikiano na malezi mazuri ambayo yalifundisha kumtumikia Mungu pamoja na Wanadamu.
 
Amewasihi Wanajumuiya ya Uru Seminari kuendeleza umoja na kuhakikisha unakuwa wenye tija kwa Taifa, pamoja na kuendelea kuiombea nchi na Viongozi wake.
 
Ibada ya Misa Takatifu ya Wanajumuiya wa Uru Seminari, imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, Mhashamu Joseph Mlola.
 
Akitoa mahubiri kwa Wanajumuiya wa Uru Seminari , Askofu Mlola amewasihi kukumbuka wito muhimu walionao wa kupeleka tunu njema ya Maisha ya kiimani kuishi kwa kumpendeza Mungu pamoja na wanadamu. Amesema ni muhimu kuwa mstari wa mbele kupeleka matumaini, ukweli, amani na haki.
 
Pia, Askofu Mlola amewasihi kuhakikisha uwepo wa kila mwanajumuiya wa Uru Seminari analeta upendo na matumaini, kwa kutambua huo ni wito kwao waliolelewa na kufundishwa katika malezi na maadili mema.
 
Uru Seminari ni Shule inayomilikiwa na Shirika la Mitume wa Yesu chini ya Kanisa Katoliki  Jimbo Moshi Mkoani Kilimanjaro.











Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments

Na: Mwandishi Wetu
Mpango wa serikali wa kutoa mikopo isiyo na riba ya asilimia kumi kwa wanawake, vijana na wenye mahitaji maalum, imeonyesha kuzaa matunda kwa wananchi wa Mbalizi mkoani Mbeya.

Hii ni kutokana wa wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo ya kujikwamua kiuchumi na kubadili hali za maisha yao.

Matokeo chanya hayo yameonekana katika ziara ya Wajumbe wa Baraza la Utekelezaji la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Mary Chatanda, Agosti 6, 2026.

Akiwa katika ziara hiyo, Chatanda ametembelea kikundi cha wauzaji wa nafaka ambacho kimenufaika na mkopo wa shilingi milioni 56. Kikundi hicho kimefanikiwa kurejesha robotatu ya mkopo huo. Kutokana na uaminifu huo, Chatamda ameeleza wakimaliza mkopo huo, wakopeshwe tena kwa kuwa wamefanya vizuri katika marejesho ya mkopo wao.

"Mmefanya vizuri kukopa ili mjikwamue kiuchumi, na kwa kuwa mmefanikiwa kurejesha robotatu ya mkopo wenu, nitoe wito kwa uongozi wa Halmashauri kuwakopesha tena pindi mtakapomaliza mkopo wenu wote, na mimi nawachangia 1,200,000 ili mlipe pango kwa kipindi cha mwaka mzima," amesema Chatanda.

Vilevile, ujumbe wa UWT Taifa, ulitembelea kikundi cha mamalishe cha stendi ya Mbalizi ambacho kimekopeshwa milioni 50. Kikundi hicho kimeendelea kurejesha vizuri mkopo wao na kufanikisha kuzalisha biashara nyingine.

Halikadhalika, wamewatembelea wanawake wauzaji wa matunda katika stendi hiyo, ambapo Chatanda aliwapa elimu ya ujasiriamali na kuwachangia 300,000 ili iongeze mtaji katika biashara yao.





 

Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments

Na Mwandishi wa OTR
Dar es Salaam. Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara na Maendeleo (TDB), Bw. Admassu Tadesse, kuhusu namna benki hiyo inavyoweza kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha ufanisi wa uwekezaji wa Serikali.

Mazungumzo hayo yana umuhimu wa kipekee kwa Tanzania kwa kuzingatia kwamba Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inamiliki asilimia 8.3 ya hisa katika TDB na hivyo kuwa miongoni mwa wanahisa wa benki hiyo ya maendeleo ya kikanda.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam yalijikita katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo namna TDB inavyoweza kuongeza mchango wake katika maendeleo ya Tanzania na kuimarisha ufanisi wa uwekezaji wa Serikali.

Bw. Mchechu alisema ushirikiano kati ya Tanzania na TDB ni muhimu katika kuendeleza uwekezaji, biashara na upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya miradi yenye mchango katika maendeleo ya uchumi.

Alisema TDB, kama taasisi ya fedha ya maendeleo ya kikanda, ina nafasi muhimu katika kusaidia Tanzania kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali na kuongeza thamani ya uwekezaji wa umma unaosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, wenye thamani ya Sh92.3 trilioni.

Bw. Mchechu alisema Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kuboresha utendaji wa taasisi za umma, huku akisisitiza uwajibikaji, ufanisi, uongozi wenye ufanisi na matumizi bora ya rasilimali za umma.

Alisema mageuzi hayo yanaenda sambamba na juhudi za kuhakikisha taasisi na kampuni zinazomilikiwa na Serikali zinafanya kazi kwa ufanisi zaidi, zinatimiza malengo ya kuanzishwa kwake na kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Bw. Tadesse alisema TDB iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kusaidia juhudi za maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji.

Alisema benki hiyo imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kutoa masuluhisho mbalimbali ya kifedha, ikiwemo ufadhili wa kibiashara, fedha za masharti nafuu na mifumo ya ufadhili mseto, kwa ajili ya kusaidia miradi yenye mchango katika maendeleo.

Bw. Tadesse alisema TDB inaiona Tanzania kama nchi yenye fursa kubwa za uwekezaji na ambayo inaendelea kuchukua hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wake.

Alisema benki hiyo inalenga kuelekeza mtaji katika nchi na miradi ambayo inaweza kuleta matokeo ya kiuchumi, kijamii na kifedha, huku ikisaidia kuongeza uzalishaji, biashara na uwekezaji.

Alisema benki hiyo imekuwa ikishirikiana na washirika mbalimbali wa maendeleo katika kuandaa mifumo ya ufadhili inayoweza kusaidia miradi yenye umuhimu wa maendeleo, hasa katika maeneo ambayo bado hayajafikia kiwango cha kuvutia mitaji ya kibiashara kwa kiwango kikubwa.

Mshauri wa TDB, Bw. Anthony Mwithiga, alisema benki hiyo imeendelea kujenga mifumo mbalimbali ya ufadhili inayolenga kuziba mapengo ya mitaji na kusaidia miradi yenye umuhimu wa kiuchumi na kijamii.

Bw. Mwithiga alisema TDB inaweza kutumia uzoefu wake katika kuunganisha vyanzo mbalimbali vya fedha, ikiwemo mitaji ya kibiashara, fedha za masharti nafuu na rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo, kulingana na mahitaji na aina ya mradi.
Posted by MROKI On Saturday, August 08, 2026 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo