Nafasi Ya Matangazo

April 23, 2024

Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akishiriki katika maandamano ya amani kuelekea uzinduzi wa Jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi Kata ya Kiwangwa, Tarafa ya Msata. 
Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akishiriki katika maandamano ya amani kuelekea uzinduzi wa Jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi Kata ya Kiwangwa, Tarafa ya Msata.
Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati wa 25 uzinduzi wa Jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi Kata ya Kiwangwa, Tarafa ya Msata
Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amezindua Jukwaa la kuwezesha wanawake kiuchumi Kata ya Kiwangwa, Tarafa ya Msata. 

Sherehe hizo zilizopambwa na maandamano ya Amani yakifuatiwa na mjadala kuhusu uwezeshaji na fursa mbalimbali za kumkomboa na kumuwezesha Mwanamke katika jamii.

Kikwete alisema kupitia fursa mbalimbali zilizopo zikiwemo za ndani ya Halmashauri na zile zinazo simamiwa na Serikali kuu wanawake wana nafasi ya kusaidia ukuaji wa kipato ndani ya jamii na familia.

 "Kwa mujibu wa Taarifa za Sensa, ongezeko wa idadi ya Wanawake wanaotegemewa ndani ya Familia umeongezeka  kufikia asilimia 37.6. Idadi hii inatoa fursa za kuwezesha wanawake katika jamii," alisema Kikwete.  

Aidha alisema Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kurudisha mikopo ya asilimia 10, mfuko kusaidia Wananchi kuendelea kutenga fedha kuwezesha wananchi kiuchumi na fursa nyenginezo. 

Kikwete ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze aliwaunga mkono kupitia ofisi ya Mbunge ambayo ilichangia Shilingi Milioni 4.6 kuwezesha vikundi kukopeshana.
Posted by MROKI On Tuesday, April 23, 2024 No comments
 




Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora Ndg. Ridhiwani Kikwete amewataka WAHITIMU wa kidato cha sita katika shule ya Kati ya Lugoba , Halmashauri ya Chalinze  Mkoani Pwani kufanya vizuri katika mitihani yao.

Kikwete ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze ameyasema hayo wakati  akihutubia wahitimu wa kidato cha Sita katika mahafali shuleni hapo leo.

Kikwete aliwaasa wahitimu hao kuhakikisha wanafaulu ili waache deni la kufuatwa na wadogo zao wanaowafuata kwa upande mmoja, wawape heshima Walimu na wazazi pia kwa kufaulu vizuri.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mbunge kuzungumza na Wahitimu, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Sakasa aliishukuru serikali kwa kuendelea kupeleka pesa za Elimu bure , vifaa na kuongezeka kwa madarasa na walimu shuleni hapo huku akimuomba Mgeni rasmi kuendelea kuikumbuka shule hiyo kwa kuisaidia vifaa na kuongeza mabweni ya wanafunzi. 
Posted by MROKI On Tuesday, April 23, 2024 No comments
Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akishiriki zoezi la usafi katika Soko Kuu la Mji wa Singida akiwa na Wananchi wa Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza na Wakazi wa Mji wa Singida mara baada ya kumaliza shughuli za usafi katika Soko Kuu la Singida ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mkuu wa wilaya ya Singida Godwin Gondwe  akifanya usafi na wananchi katika soko kuu la Singida.
Mkuu wa wilaya ya Singida Godwin Gondwe akizungumza na wakazi wa mji wa Singida kabla ya kumkaribisha Mkuu wa mkoa Kuzungumza na Wakazi wa Mji wa Singida walioshiriki zoezi la Usafi.


Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego akishiriki zoezi la usafi katika Soko Kuu la Mji wa Singida akiwa na Wananchi wa Singida.

Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego ameonya kuwa atawachukulia hatua kali watu au kikundi cha watu wanaotaka kuvuruga au kuvunja amani na utulivu kwa wananchi wa mkoa wa Singida.

Mkuu wa mkoa wa Singida ametoa kauli hiyo (leo 23/Apr/24 ) mjini Singida, katika uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Soko Kuu la Singida.

Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amewasisitiza wananchi wa mkoa wa Singida kuwakataa watu au mtu yeyote anayetaka kumdhalilisha Rais au Watanzania kwani wakiwaruhusu kufanya hivyo watakuwa wamedhalilisha Taifa na Watanzania wote hivyo ni lazima wananchi wote waungane kukataa watu hao wenye nia mbaya na Taifa la Tanzania.

“Tuungane wote katika kupambana na yeyote anayetaka kuleta ujinga ujinga katika Taifa letu tuwabaini ili tuwawajibishe “ Amesisitiza Halima Dendego.

Halima Dendego amesema yeye ni rafiki wa wote Vijana,Wazee na Wanawake hivyo Ofisi yake ipo wazi muda wote kwa anayetaka kusaidiwa kwa shida yeyote aende ili asaidiwe nia ni kuona wananchi Singida wanaishi maisha mazuri na yenye staha bila kero. 

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Singida Godwin Gondwe amemhakikishia Mkuu wa mkoa wa Singida kuwa atasimamia maelekezo yake yote aliyotoa hasa ya kuhakikisha Manispaa ya Singida inakuwa safi katika maeneo yote ya Masoko na maeneo yenye watu wengi kama hatua ya kudhibiti magonjwa ya maambukizi ikiwemo kipindupindu.

Godwin Gondwe amesema kuwa hivi karibuni watazindua kampeni kubwa ya usafi katika Manispaa ya Singida ambayo itasaidia kuboresha usafi katika maeneo yote ya mji wa Singida ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida Edward Mboya amebainisha kuwa kupitia mapato ya ndani wanaendelea na mchakato wa kununua gari nyingine mpya ya kubebea taka na vifaa vya kuhifadhi taka lengo ikiwa ni kuifanya Manispaa ya Singida kuwa bora nchini hasa katika masuala ya Usafi.


 Mkuu wa wilaya ya Singida Godwin Gondwe akizungumza na wakazi wa mji wa Singida kabla ya kumkaribisha Mkuu wa mkoa Kuzungumza na Wakazi wa Mji wa Singida walioshiriki zoezi la Usafi.
Posted by MROKI On Tuesday, April 23, 2024 No comments

April 22, 2024







Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde leo Aprili 22, 2024 jijini Dodoma amekutana na wafanyabiashara wa madini na wachimbaji wa madini kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili kwenye shughuli zao ikiwemo changamoto ya ukosekanaji wa teknolojia ya uchenjuaji wa baadhi ya madini na hivyo kuielekeza Tume kuandaa utaratibu sahihi wa usafirishaji wa madini yaliyongezwa thamani kwa kiwango cha teknolojia inayopatikana hapa nchini.

Ametoa maelekezo hayo, mara baada ya kusikiliza changamoto za wafanyabiashara wa madini na wachimbaji wa madini ikiwemo zuio la kusafirisha madini ghafi lililotolewa na Serikali mapema mwaka 2017 ambapo wameomba Serikali kuwapa muda wa kusafirisha madini yaliyoongezwa thamani kwa kiwango cha teknolojia inayopatikana nchini kwa sasa kutokana na kutokuwepo kwa viwanda vya kuchenjua madini hayo hali iliyowasababishia kuendesha shughuli zao kwa hasara.

“Naielekeza Tume ya Madini kuweka utaratibu maalum wa usafirishaji wa madini hayo kwa kipindi cha mpito cha mwaka mmoja wakati mkijipanga kuhakikisha madini yanachenjuliwa ndani ya nchi kwa kiwango kikubwa” amesema Mavunde.

Amesema kuwa, lengo la Serikali la kuweka mkazo wa kuyaongezea thamani madini yote nchini ni kuongeza faida kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini huku Serikali ikipata kodi zaidi, hivyo Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango kwenye Pato la Taifa.

Aidha, amewataka wadau wa madini kuwekeza kwenye viwanda vya uchenjuaji wa madini sambamba na kuwakaribisha wawekezaji kutoka nje ya nchi kwenye ujenzi wa viwanda  hivyo na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda vya kuchenjua madini nchini.

“Muda wote milango ya ofisi yangu ipo wazi kwa mwekezaji yeyote mwenye nia ya kuwekeza kwenye kiwanda cha kuongeza thamani  madini nchini, tunataka kuhakikisha Serikali inapata kodi zaidi fedha ambazo zinatumika kwenye uboreshaji wa  huduma za jamii kama vile barabara, maji, vituo vya afya sambamba na kufungua fursa za ajira huku wadau wa madini wakiendelea kutajirika,” amesisitiza Waziri Mavunde.

Katika hatua nyingine amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na sheria na kanuni bora za madini, miongozo mbalimbali, kodi na tozo rafiki ili kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Ameongeza mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuendelea kufanya tafiti mbalimbali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na uanzishaji wa maabara ya kisasa ili kuhakikisha wachimbaji wa madini wanaendesha shughuli zao kwa uhakika na kutajirika.

“Kama Wizara ya Madini kupitia Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri tumeweka lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 utafiti wa kina wa madini nchini (high resolution) uwe umefikia asilimia 50 kutoka asilimia 16 ya sasa; mpaka sasa tumeshafanya tafiti katika maeneo ya Dodoma, Geita, Kahama, Mirerani, Lindi na Mtwara,” amesema Mavunde.

Awali akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amesema kuwa lengo la kikao hicho lilikuwa ni kusikiliza kero za wafanyabiashara na wachimbaji wa madini na kuzitatua sambamba na kutoa ufafanuzi katika maeneo mbalimbali yahusiyo Sekta ya Madini.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Kamishna wa Madini Nchini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba na menejimenti na watumishi kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.
Posted by MROKI On Monday, April 22, 2024 No comments



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaajiri walimu wapya wa masomo ya sayansi na itaendelea kuboresha maslahi yao.

Rais Dk.Mwinyi amesema hayo alipofungua Skuli ya ghorofa ya Sekondari Hassan Khamis Hafidh iliopo Monduli, Wilaya ya Magharibi A , Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe 22 Aprili 2024 ikiwa ni shamrashamra za Miaka ya 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. 

Aidha Rais Dk.Mwinyi amewapongeza Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri ya kuvuka malengo ya ilani ya utekelezaji ya uchaguzi ya CCM 2020-2025.

Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa ujenzi wa  miundombinu ya Skuli ina lengo la kuboresha ili kupunguza msongamano wa wanafunzi na kutozidi idadi ya 45 kila darasa.

Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amewataka wananchi kuendelea kuudumisha Muungano ili kupata maendeleo katika nyanja zote.
Posted by MROKI On Monday, April 22, 2024 No comments







Na John Mapepele
Serikali imesema Tanzania inaongoza kwa kuwa na Simba, Nyati na Chui wengi katika bara la Afrika huku ikishirikilia nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa yaTembo.

Hayo yamesemwa leo Aprili 22, 2024 kwenye mkutano ambao Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki ametangaza rasmi matokeo ya Sensa ya Wanyamapori na kuzindua taarifa ya Watalii wa Kimataifa walioitembelea Tanzania mwaka 2023.

Sensa hiyo ya wanyamapori imefanywa na TAWIRI kwa kushirikiana na TANAPA, TAWA, NCAA, Idara ya Wanyamapori, na Frankfurt Zoological Society katika mifumo ya ikolojia ya Nyerere-Selous-Mikumi,Saadani-Wamimbiki na Serengeti 

Mkutano huo uliwahusisha wadau wa uhifadhi na utalii, ambapo Mhe. Kairuki amesema tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya sensa ya wanyamapori nchi nzima mapema hapo mwakani.

 Aidha, Mhe. Kairuki amesema matokeo ya sensa hiyo yatasaidia kwenye usimamizi wa wanyamapori nchini na kupanga mipango mbalimbali ya kuboresha  uhifadhi na  kutangaza  utalii duniani.

Mhe. Kairuki ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana na Serikali ambapo ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI) kuandaa mpango kazi kwa ajili ya sensa ijayo huku pia akielekeza watendaji wa wizara yake kuchambua kwa kina  matokeo ya sensa hii  ili yaweze kuleta tija.

Akitoa taarifa ya sensa hiyo amesema spishi zilizoonyesha idadi kubwa ni pamoja na Nyati (59,878), Tembo (20,006), Nyumbu (19,060), Kongoni (18,361), swalapala (14,031) na Ngiri (13,806), ambapo spishi zilizoonyesha idadi ndogo ni pamoja na Twiga (1,679), Tandala mkubwa/ kudu (1,414) na puku/sheshe (496). 

Amefafanua kuwa kwa upande wa Tembo, idadi imeongezeka kutoka 15,501 (2018) hadi 20,006 (2022) na Viashiria vya ujangili wa tembo au vifo vya tembo vimepungua kwa kiasi kikubwa hadi 0.8% mwaka 2022 ikilinganishwa na 16% wakati wa sensa ya 2018. 

Akizungumzia kuhusu taarifa ya Watalii wa Kimataifa walioitembelea Tanzania mwaka 2023 amesema Sekta ya Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa dunia na umeendelea kuimarika baada kuathiriwa na mlipuko wa janga la UVIKO-19. Mwaka 2023 sekta ya utalii duniani imeimarika kwa kiwango cha asilimia 88 ikilinganishwa na kiwango cha juu kilichofikiwa mwaka 2019.

 “Hali hii ilitokana na ukuaji endelevu wa maendeleo ya teknolojia na juhudi za kukuza na kuendeleza maeneo mengine ya utalii duniani. Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watalii duniani iliongezeka kwa asilimia 34 hadi kufikia watalii bilioni 1.3 Mwaka 2023 kutoka milioni 960 Mwaka 2022”. Ameongeza

Amesema kwa Tanzania, utalii wa Kimataifa umeimarika kwa kiwango cha asilimia 118.4 Mwaka 2023 ikilinganishwa na kiwango cha juu kabla ya janga la UVIKO-19.  Aidha, idadi ya watalii wa Kimataifa iliongezeka kutoka watalii milioni 1.4 Mwaka 2022 hadi kufikia watalii milioni 1.8 Mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 24.3. 

“Hatuna budi kutambua kazi kubwa aliyoifanya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyeitangaza Tanzania kupitia filamu ya Tanzania the Royal tour”. Amesisitiza  


Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya utalii hapa Nchini, Serikali kwa kushirikiana na wadau ilifanya utafiti wa watalii wanaoondoka Nchini Mwaka 2023 kwa lengo la kupata taarifa zinazosaidia kutunga Sera na kuandaa mipango ya maendeleo ya utalii. Aidha, taarifa za utafiti huo zinasaidia serikali kuandaa akaunti za taifa (national accounts) na mizania ya malipo ya nje (Balance of Payments). 

Aidha amesema utafiti umebainisha kuwa mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kwa asilimia 33.5 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 3.4 Mwaka 2023 kutoka Dola za Marekani 2.5 bilioni zilizopatikana Mwaka 2022.  Aidha, wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliongezeka hadi kufikia Dola za Marekani 250 Mwaka 2023 kutoka wastani wa Dola za Marekani 214 Mwaka 2022. 

Kwa upande wa Zanzibar, wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku ulikuwa Dola za Marekani 257 Mwaka 2023 ikilinganishwa na watani wa Dola za Marekani 218 Mwaka 2022.
Posted by MROKI On Monday, April 22, 2024 No comments






Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na wadau wa uhifadhi, Frankfurt Zoological Society (FZS) kutoka Ujerumani na Six Rivers Africa (SRA) ya Tanzania ambao wamekuwa wakiisaidia Serikali katika maeneo mbalimbali ya uhifadhi ikiwemo urejeshaji wa wanyama waliotoweka (restoration),utafiti, kupambana na ujangili na kusaidia jamii kujikwamua kiuchumi hasa zinazoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi pamoja na masuala ya utalii.

Kikao hicho kimefanyika leo Aprili 22,2024  katika ukumbi wa hoteli ya Gran Melia jijini Arusha.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kairuki ameendelea kuwaomba ushirikiano katika uhifadhi ikiwemo ufuatiliaji wa idadi na kufanya sensa ya wanyamapori katika mifumo ikolojia mingine ambayo muda wa sensa ya wanyamapori umechelewa akitolea mfano wa ikolojia za Burigi-Chato, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Malagarasi-Moyowosi-Kigosi na Serengeti.


Pia, amewaomba wadau hao kushiriki katika kujengea uwezo wahifadhi hasa kuhusu maendeleo ya teknolojia katika kufanya sensa ya wanyamapori na kununua vifaa vilivyoboreshwa vya ufuatiliaji wa wanyamapori na kutoa ufadhili katika tafiti za aina muhimu za Wanyamapori wakiwemo Faru, Tembo, Wanyama Wanyama Wakubwa (Simba, Chui, mbwa mwitu).

Katika hatua nyingine, amewaomba ushirikiano katika kuimarisha teknolojia kwenye kupunguza mwingiliano baina ya Binadamu na Wanyamapori ili kupunguza madhara yanayotokea kwa wananchi, kusaidia katika zoezi la urejeshaji wa shoroba za wanyamapori na kuimarisha teknolojia katika ufugaji nyuki katika maeneo yanayozunguka Hifadhi za Serengeti na Nyerere kwa ajili ya maisha ya jamii na kuboresha miundombinu (nyumba, doria barabara na viwanja vya ndege).

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amewashukuru wadau hao kwa namna ambavyo wamejitolea katika uhifadhi na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uhifadhi wanayoiendesha.

Wadau hao kwa nyakati tofauti wamesema wanaunga mkono juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uhifadhi, utafiti na kuboresha maisha ya jamii zinazopakana na Hifadhi.

FZS na SRA wamekuwa wakisaidia shughuli za uhifadhi wa Faru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba Grumeti-Ikorongo, Pori la Akiba la Maswa na Hifadhi ya Ngorongoro, ufuatiliaji wa idadi ya wanyamapori (sensa) katika mfumo ikolojia wa Serengeti na mfumo wa ikolojia wa Selous-Nyerere-Mikumi na kusaidia shughuli za Utafiti.
Posted by MROKI On Monday, April 22, 2024 No comments

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ya kumuombea marehemu Mwanachuoni Alhabyb Ahmad Bin Abuubakar Bin Sumeit ikisomwa na Sayy Mudh-hiridin Ally Qullatein (kushoto kwa Rais)  wakiwa katika kaburi la marehemu lililoko katika eneo la  Msikiti wa Ijumaa Malindi Wilaya Mjini Unguja, wakati wa hafla ya Hauli ya 102 iliyofanyika leo 22-4-2024 na (kushoto kwake) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman na Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akijumuika na Masheikh na Wananchi mbalimbali katika Kisomo cha Hauli ya 102 ya kumuombe Marehemu Mwanachuoni Mkubwa Alhabyb Ahmad Bin Abuubakar Bin Sumeit, iliyofanyika leo 22-4-2024 katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Malindi Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar na (kushoto kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe.Haroun Ali Suleiman na (kulia kwa Rais) Sheikh. Sayy Mudh-hiridin Ally Qullatein.

AYY.Omar Bin Ally Qullatein akihitimisha kisomo cha Hauli ya 102 ya kumuombea Marehemu Mwanachuoni Mkubwa Zanzibar Alhabyb Ahmad Bin Abuubakar Bin Sumeit, iliyofanyika leo 22-4-2024 katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Malindi Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar, na (kushoto kwake) Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Khalid Ali Mfaume.
WAUMINI wa Dini ya Kiislam wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza na kuwasilimia Masheikh na Wananchi baada ya kumalizika kwa Kisomo cha hitma na dua (hauli ya 102 tangu kufariki kwake) ya kumuombea Mwanachuoni Mkubwa Zanzibar Alhabyb Ahmad Bin Abuubakar Bin Sumeit,iliyofanyika leo 22-4-2024 katika msikiti Mkuu wa Ijumaa Malindi Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akijumuika na Masheikh na Wananchi katika kuitikia dua ya kumuombea Mwanachuoni marehemu Alhabyb Ahmad Bin Abuubakar Bin Sumeit,ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi (kushoto kwa Rais) baada ya kumalizika kwa kisomo hicho kilichofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Malindi Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar leo 22-4-2024.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Sheikh. Ali Hemed Jabir (Aliyani) baada ya kumalizika kwa Hauli ya 102 na dua ya kumuombea Mwanachuoni marehemu Alhabyb Ahmad Bin Abuubakar Bin Sumeit,iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Malindi Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar leo 22-4-2024.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Masheikh, Wanavyuoni na Wananchi baada ya kumalizika kwa Hauli ya 102 na dua ya kumuombea Marehemu Alhabyb Ahmad Bin Abuubakar Bin Sumeit,iliyofanyika leo 22-4-2024 katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Malindi Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar.

Posted by MROKI On Monday, April 22, 2024 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo